Mtandao wa Yahoo umethibitisha kuwa wadukuzi wamedukua taarifa za zaidi ya watumiaji milioni mia tano katika akaunti zake za watumiaji.
Hata hivyo Yahoo imesema inaamini kuwa shambulio la kimtandao la mwaka 2014 lilikuwa limefadhiliwa na serikali.
Data zilizoibwa ni pamoja na majina, anuani za barua pepe, namba za simu, tarehe za kuzaliwa na nywila za watumiaji ama (Password). Lakini wadukuzi hao hawakugusa kadi za malipo na taarifa za akaunti za kibenki.
Watumiaji wa mtandao huo wameshauriwa kubadilisha nywila zao (password) zao ili kuepuka udukuzi wa kimtandao.
CHANZO BBC
Friday, September 23, 2016
Madam Rita wa BSS kufilisiwa
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Udalali ya Yono, wameifungia Kampuni ya Benchmark Productions na kuipa muda wa siku 14, iwe imelipa deni la kodi ya Sh bilioni 7.04, vinginevyo mali za kampuni hiyo zitauzwa kwa mnada.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Meneja Msaidizi wa Madeni wa TRA, Mkoa wa Kinondoni wa Kodi, Sylver Rutagwelera alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuidai kampuni hiyo inayomilikiwa na Rita Paulsen kwa muda mrefu bila kulipa.
TRA, wakiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono, walifika eneo la Mikocheni jijini hapo jana asubuhi ziliko ofisi za kampuni hiyo na kuwaeleza wahusika kuhusu deni hilo, na kuwataka waoneshe risiti za malipo iwapo wameshaanza kulipa deni hilo, jambo ambalo wahusika hao hawakuwa nazo.
Hata hivyo Meneja Operesheni wa Kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Evelyn alifika ofisini hapo na kuwaambia maofisa hao kuwa walishaanza mawasiliano jinsi ya kulipa deni hilo. “Zipo barua tulizokuwa tumeanza kufanya mawasiliano na TRA, kuhusu deni hili, lakini pamoja na hayo, deni lenyewe ni kubwa kuliko uwezo wa kampuni,” alisema Evelyn.
Hata hivyo Rutagwelera alisema mmiliki wa kampuni hiyo anadaiwa kodi tangu mwaka 2009 na alikuwa akitumia jina lingine kwenye kampuni hiyo na baada ya muda aliifunga na kufungua hiyo ya Benchmark ili hali deni la nyuma hajalipa.
“Mdaiwa huyo alikuwa ana kampuni aliyoipa jina lingine na tulimkumbusha kulipa kodi ya serikali tangu mwaka 2009 ila hakutekeleza na badala yake aliamua kuifunga kampuni na kufungua hii, akidhani deni limefutika”, alisema Rutagwelera.
Alisema baada ya kuona muda unasonga na deni linazidi kuongezeka bila mdaiwa kuonesha juhudi za kulipa waliamua kukabidhi mdaiwa huyo kwa Kampuni ya Yono kwa ajili ya kufuatilia deni hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela alisema wameifungia kampuni hiyo na kuanzia sasa walinzi wa Yono watalinda na baada ya muda wa siku 14, waliopewa kulipa deni hilo ukipita, watachukua hatua nyingine kisheria ya kuuza mali za kampuni hiyo kwa mnada.
Alisema deni hilo ni kubwa kwa sababu ni muda mrefu umepita kodi ya serikali haijalipwa na kuwashauri Watanzania kuacha tabia ya kulimbikiza kodi kwa sababu deni litakuwa kubwa ila likilipwa kwa wakati linaondoa usumbufu usio wa lazima.
“Yono tumepewa kazi ya kukusanya madeni ya serikali na tutaendelea kuwakamata wale wote tunaopewa kuwafuatilia lengo sio kuwaumiza ni kuhakikisha kodi ya serikali inakombolewa kwa manufaa ya nchi yetu, kwa maana tunamuunga mkono Rais John Magufuli kuhakikisha taifa letu linaendelea kwa kukusanya mapato stahiki”, alisema Kevela.
CHANZO HABARILEO
Monday, September 19, 2016
Binti wa Donald Trump agwaya maswali mazito ya mwanahabari
![]() |
Binti wa Donald Trump, mgombea uraiswa Marekani kwa tiketi
ya Chama cha Republican, Ivanka Trump
|
BINTI wa Donald Trump, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, Ivanka Trump, amelazimika kusitisha mahojiano na gazeti la Cosmopolitan linalochapwa baada ya kuulizwa maswali magumu.
Maswali hayo yanahusu kauli mbalimbali za baba yake huyo alizowahi kutamka kuhusu masuala ya afya ya watoto na likizo ya wazazi.
Badala ya kujibu maswali, binti huyo alimlaumu mwanahabari aliyekuwa akimhoji kwa madai kwamba maswali hayo yamegubikwa na “mambo mengi hasi”.
Binti huyo alikuwa akitaraji kuulizwa kuhusu sera mpya ya afya ya watoto ya mgombea wa Republican Donald Trump, ambayo alisaidia kuiandaa na kuitangaza rasmi wiki hii.
Mwanahabari, Prachi Gupta alimuhoji binti huyo akisema; “Mwaka 2004 Donald Trump alisema kwamba mimba ni kitu kibaya kwa biashara. Inashangaza kuona sera hii kutoka kwake leo. Unaweza kuzungumzia matamshi hayo na labda ni kitu gani kimebadilika?”
Binti huyo hakuzubaa akajibu; “Sasa nadhani una mambo hasi sana kwenye haya maswali. Kwa mujibu wa gazeti la Cosmopolitan Ivanka akaendelea kulaumu akisema; “Kwa hiyo sifahamu ni kwa kiasi gani inasaidia kutumia muda mwingi na wewe kuhusu hili, kama unatoa matamshi kama hayo.”
Gupta aliendelea; “Ningependa kusema kwamba samahani kwa maswali – unayoyaona kwamba ni hasi. Lakini hayo maswali yana maana kwamba mgombea urais alitoa hayo matamshi wakati fulani. Kwa hiyo mimi nimekuwa nikifuatilia tu.”
Ivanka akajibu; “Ahaa, umesema kwamba alitoa hayo matamshi. Mimi sifahamu kama aliwahi kuyatoa.
Alipooneshwa chanzo cha nukuu ya baba yak ambacho ni ya Donald Trump na Shirika la Habari la NBC mwaka 2004, binti huyo akawa mkali zaidi .
Hasira za binti huyo zilikuwa dhahiri mara alipoulizwa kwa nini hoja za wakati wa kampeni kuhusu likizo haziwahusishi wenza wa mashoga au haijumuishi likizo ya kina baba ya uzazi. Lakini hata hivyo alijibu kwamba sababu ni kuwa “…nia halisi ya mpango ni kuwasaidia kina mama kupona.”
Mwandishi akauliza; “Kwa hiyo nataka kuweka hili sawa, kwa wapenzi wa jinsia moja ambao wanaokubali watoto kuwa wao, ambapo wazazi hao wawili wote ni wanaume, hawatapata likizo maalumu kwa sababu hawahitaji kupona?”
Ivanka Trump akamjibu akisema: “Hayo ni maneno yako, sio yangu. Hayo ni maneno yako. Mpango kwa sasa unaaangalia kina mama zaidi, haijalishi kama watakuwa kwenye ndoa ya jinsia moja au hapana.”
Wakati Gupta alipoanza kumuuliza ni kwa jinsi gani Donald Trump ataweza kugharimia mapendekezo yake ambayo ni ghali sana – kama vile ujenzi wa ukuta kati ya mpaka wa Marekani na Mexico, uwekezaji katika miundombinu na kuongeza matumizi ya kijeshi, Ivanka Trump alijibu kuwa mipango hiyo itagharimiwa na mpango mkuu kabambe wa mageuzi ya kodi kwa nchi hiyo.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya hapo alifanya uamuzi ‘mgumu’ wa kusitisha mahojiano hayo. “Naondoka – nalazimika kuondoka. Samahani,” alitamka.
Baadae kwa kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ivanka Trump aliandika, “Cosmopolitan, wasomaji wenu wanajali na wanapaswa kujali kuhusu masuala yanayoawaathiri kina mama na watoto. Weka malengo panapostahili – simamia mabadiliko.”
Mtafaruku huo unajitokeza katika wakati ambao tayari timu ya kampeni ya Hillary Clinton, mgombea wa Democrat ikishutumu mpango huo wa Donald Trump kwa madai kwamba ‘unawaangalia’ kina mama pekee na kuwasahau kina baba.
Imeandikwa na CNN na kutafsiriwa na mwandishi wa Raia Mwema
Tanzania bora duniani huduma za simu na fedha mtandaoni

Hayo yalibainishwa katika mkutano wa kimataifa wa sita wa kujadili namna ya kuboresha zaidi huduma za simu na fedha kwa njia ya mtandao, ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akifungua mkutano huo Dar es Salaam leo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, amesema tangu kuanza kwa matumizi ya huduma za simu na fedha kwa njia ya mtandao mwaka 2008, Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.
Kwa habari zaidi soma Habarileo Septemba 20.
CHANZO: http://www.habarileo.co.tz/
Subscribe to:
Comments (Atom)